DEREVA wa gari dogo lililowagonga watu waliokuwa wakifanya mazoezi ya kukimbia na kuwaua sita amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ilemela mkoani hapa.
Kijana huyo Oswald Binamungu (39), mkazi wa Kata ya Buswelu wilayani Ilemela anadaiwa kuwagonga kwa nyuma watu hao Julai 22, mwaka huu muda wa saa 12:30 asubuhi.
Katika ajali hiyo, inadaiwa kuwa wakati Binamungu anaendesha gari aina ya Toyota Hilux Double Cabin lenye namba za usajili T476 DZL alijeruhi watu tisa katika eneo la Kiseke.
Watu hao waligongwa wakati kikundi cha mazoezi cha Hoteli ya Added Palace ya jijini Mwanza kikifanya mazoezi ya kukimbia.
Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Anita Mweli alieleza mahakama kuwa Binamungu anashtakiwa kwa kuendesha gari kwa mwendokasi uliosababisha vifo na madhara.
Mweli aliwataja waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo ni Selestine Daudi, Shadrack Safari, Peter Fredrick, Makongoro Manyanda, Nehemia Hamis na Aman Matinde.
Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Masanja Magnus, Godfrey Benard, Simikiwa Peter, Mathias Patrick, Mashaka Maulid, Steven Tweve, Ponasian Remigius, Grace Chacha na Baraka Nehemia.
Mweli alieleza kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilemela, Amani Sumari alisema mashitaka yanayomkabili Binamungu yanaweza kupata dhamana.
Sumari alitaja masharti ya dhamana kuwa ni wadhamini wawili na moja ya wadhamini hao anatakiwa awe mtumishi wa umma na kila mdhamini atasaini dhamana ya Sh milioni 10.
Kesi hiyo namba 27 ya mwaka 2023 itasomwa tena Agosti 10, mwaka huu.